Taarifa za Utabiri
TAHADHARI ya upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayozidi mita 2 imetolewa kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wote wa pwani ya bahari ya Hindi (mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Lindi, Mtwara, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba)
MWELEKEO WA MVUA KWA TAREHE 11-20 JANUARI, 2025
Kanda ya ziwa Viktoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara): Vipindi vya mvua zinazoambatana na ngurumo za radi vinatarajiwa katika maeneo machache.
Nyanda za juu kaskazini-mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro): Vipindi vya mvua nyepesi vinatarajiwa katika maeneo machache.
Pwani ya kaskazini (Mikoa ya Tanga, Maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, Pwani na Dar es Salaampamoja na visiwa vya Unguja na Pemba): Vipindi vya mvua vinatarajiwa katika maeneo machache.
Magharibi mwa nchi (Mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora): Mvua zinazoambatana na ngurumo za radi zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo.
Kanda ya kati (Mikoa ya Dodoma na Singida): Vipindi vya mvua vinatarajiwa katika maeneo machache hususan katika kipindi cha nusu ya kwanza ya dekadi.
Nyanda za juu Kusini-magharibi (Mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa): Mvua zinazoambatana na ngurumo za radi zinatarajiwa katika maeneo machache.
Pwani ya kusini (Mikoa ya Mtwara na Lindi): Vipindi vya mvua vinatarajiwa katika maeneo machache.
Kanda ya kusini (Mkoa wa Ruvuma na Maeneo ya kusini mwa Morogoro): Mvua zinazoambatana na ngurumo za radi zinatarajiwa katika maeneo machache.
Imetolewa na;
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
Kwa maelezo zaidi tafadhali pakua...
Dondoo za tathmini ya Desemba, 2024 na mwelekeo wa Januari, 2025:
Taarifa hii inatoa muhtasari wa mifumo ya hali ya hewa pamoja na mwenendo wa hali ya hewa kwa mwezi Desemba, 2024 na kutoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa mwezi Januari, 2025 nchini.
- Katika kipindi cha mwezi Desemba, 2024 baadhi ya maeneo nchini yalipata mvua za wastani. Aidha, vipindi vya mvua kubwa vilijitokeza katika baadhi ya maeneo na kusababisha athari ikiwemo mafuriko na kutuama kwa maji.
- Katika kipindi cha mwezi Januari 2025, mvua zinatarajiwa kuendelea katika maeneo mengi yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka ikiashiria muendelezo wa mvua za Msimu. Hata hivyo, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Aidha, ongezeko la mvua linatarajiwa katika baadhi ya maeneo.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali pakua
Dondoo muhimu za mvua za Msimu (Novemba, 2024 – Aprili, 2025)
Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (kanda ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo yaliyopo kusini mwa mkoa wa Morogoro) katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2024 hadi Aprili, 2025. Ushauri na tahadhari umetolewa kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya, sekta binafsi pamoja na menejimenti za maafa. Muhtasari wa mwelekeo wa mvua hizo na athari zake ni kama ifuatavyo:
a) Mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:
(i) Mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida na Dodoma; kaskazini na mashariki mwa mkoa wa Lindi, na kaskazini mwa mikoa ya Mbeya na Iringa. Aidha, mvua za Wastani hadi Juu ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara, maeneo ya kusini na magharibi mwa mkoa wa Lindi, kusini mwa mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro.
(ii) Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2024 katika mkoa wa Kigoma na kusambaa katika maeneo mengine yanayopata mvua za Msimu mwezi Novemba, 2024 na mwisho katika mkoa wa Ruvuma Disemba, 2024.
(iii) Kipindi cha nusu ya pili ya msimu (Februari – Aprili, 2025) kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi ikilinganishwa na nusu ya kwanza (Novemba, 2024 – Januari, 2025).
b) Athari na ushauri
(i) Shughuli za kilimo zinatarajiwa kuendelea kama ilivyo kawaida katika maeneo mengi katika mvua za Msimu 2024/2025. Hata hivyo, vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo, hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani.
(ii) Kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka, hali inayoweza kusababisha mafuriko, hasa katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko.
(iii) Jamii zinazokaa katika maeneo yenye hatari ya mafuriko zinashauriwa kuchukua hatua stahiki.