Huduma Zetu
Hali ya hewa na mabadiliko ya hali ya hewa yanaathiri sio tu ukuaji na maendeleo ya mimea lakini pia ubora wa mavuno, ufanisi wa nyenzo za kilimo, matumizi ya pembejeo, mlipuko wa magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao na wanyama. Kutokana na uchambuzi wa taarifa za hali ya hewa; data za setelaiti; data za mazao; na utabiri, mtaalamu wa hali ya hewa kilimo anaweza kuchambua athari za hali ya hewa iliyojitokeza na inayotarajiwa kwenye mazao na mifugo na kutoa ushauri husika. Taarifa hizi zinatolewa katika Jarida la Hali ya Hewa Kilimo.
Jarida la hali ya hewa kilimo hutolewa kwa siku kumi kumi na mwezi. Vile vile Jarida maalum ambalo lina utabiri wa msimu huandaliwa na kusambazwa kwa watumiaji kabla ya kuanza kwa msimu wa vuli mwezi Septemba na Masika mwezi Februari kila mwaka. Jarida la hali ya hewa kilimo, mbali na kutoa taarifa za hali ya hewa iliyopita na inayotarajiwa vile vile hutoa ushauri kwa wakulima na wafugaji ili wachukue hatua stahiki kutokana na hali mbaya ya hewa inayotarajiwa.
Taarifa za hali ya hewa kilimo ni muhimu sana kwenye mipango na shughuli mbalimbali kwa mfano umwagiliaji ili kuhifadhi maji/nishati, kuchagua wakati unaofaa wa kutumia viuatilifu, matumizi ya mbolea, uzalishaji wa mifugo na uvuvi, nk. Jarida la Hali ya Hewa Kilimo hutolewa kwa lugha ya Kiswahili na Kingereza, na husambazwa kila baada ya siku kumi. Kwa maelezo zaidi kuhusu machapisho na taarifa za hali ya hewa kilimo bonyeza: Jarida la Hali ya Hewa Kilimo.majarida haya husambazwa pia kupitia mfumo wa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi(FarmSMS)