Habari

Imewekwa: Jan, 15 2021

WITO WATOLEWA VYOMBO VYA HABARI KURUSHA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KILA SIKU.

WITO WATOLEWA VYOMBO VYA HABARI KURUSHA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KILA SIKU.

Dar es Salaam; Tarehe 14 Januari, 2021;

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mhandisi. Godfrey Kasekenya (MB) ametoa wito kwa vyombo vya habari kuhakikisha wanawahabarisha wananchi kuhusu taarifa za hali ya hewa ya kila siku ili kuweza kujipanga na kuepukana na majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa na kusisitiza kuwa hali ya hewa ni kazi ya kisayansi na sio ya kubahatisha.

Hayo yalizungumzwa katika ziara ya Mhe. Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi iliyofanyika katika ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 14/01/2021. Lengo la ziara hiyo ni kuifahamu TMA, kazi wanazofanya na kutambua changamoto za kiutendaji ili kuweza kufanya maboresho stahiki.

“Narudia tena, vyombo vya habari vyote, suala la taarifa za hali ya hewa liwe ni suala la lazima na watoe nafasi kubwa kwaajili ya kuwahabarisha wananchi, kwani kupitia vyombo vya Habari taarifa zitaweza kuwafikia wananchi kwa wakati na kuifanya TMA itekeleze majukumu yake kwa tija. Vinginevyo TMA itakuwa inafanya kazi na taarifa zake hazitumiki na hazisaidii wananchi katika kupunguza athari za majanga kwasababu ya kutokuzifahamu”. Alizungumza Mhe. Kasekenya.

Mhe. Kasekenya aliendelea kwa kusisitiza umuhimu wa kuhifadhi data za hali ya hewa za muda mrefu katika njia ya kielektroniki ili kuweza kusaidia katika maendeleo ya nchi, huku akitoa mfano wa ujenzi wa madaraja katika maeneo yenye historia ya mvua kubwa kwa kuangalia hali ya hewa ya muda mrefu itakayosaidia kujenga madaraja imara yasiyoathiriwa na mafuriko. Aliendelea kwa kuipongeza TMA kwa kupewa majukumu ya kusaidia nchi zingine katika masuala ya hali ya hewa, hii ni kutokana na uongozi bora wa mkurugenzi mkuu Kitaifa na Kimataifa. Alisema Mhe. Kasekenya.

Mheshimiwa Naibu Waziri aliiagiza TMA kutekeleza majukumu yake kwa weledi na aliahidi katika utaratibu wa kuboresha maslahi ya watumishi kama alivyoahidi Mhe. Rais watumishi wa TMA watakumbukwa pia. Alisema Taaluma ya hali ya hewa ni kati ya taaluma ambazo ni ‘rare profession’ kwani inachukua muda mrefu kumuandaa mtaalam na mafunzo hayo yanapatikana nje ya nchi ukiacha shahada ya kwanza inayotolewa chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Awali, wakati akimkaribisha Mhe. Naibu Waziri, Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi kupitia taarifa yake fupi aliishukuru Serikali kwa uwekezaji uliofanyika katika sekta ya hali ya hewa na hivyo kuongeza usahihi wa utabiri, na kuiomba Wizara kuwezesha kufanikisha maslahi ya watumishi wa Mamlaka kwa kuwapatia mishahara iliyopendekezwa baada ya zoezi la “job evaluation” ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Mheshimiwa Naibu Waziri, kazi ambazo watumishi wa Mamlaka wanazifanya zinahitaji weledi wa hali ya juu ambapo mishahara wanayopata ni midogo, kazi hizi zinafanyika kwa saa 24 siku 7 kwa wiki bila kujali jua, mvua, upepo mkali, wanyama wakali, nyoka n.k, watumishi hutoka nje kupima taarifa za hali ya hewa kila nusu saa kwa vituo vyote vilivyopo maeneo mbalimbali nchini”. Alifafanua Dkt. Nyenzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMA na makamu wa tatu wa rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Dkt. Agnes Kijazi alimshukuru Mhe. Kasekenya kwa kutembelea TMA na kuahidi kuisaidia Mamlaka kutekeleza majukumu yake kwa weledi kwa kuendelea kuboresha mtandao wa vituo vya hali ya hewa na maslahi ya watumishi. Dkt. Kijazi aliamuahidi Mhe. Waziri kwamba maagizo yote aliyoyatoa katika ziara hiyo TMA itayatekeleza.

Aidha, aliendelea kwa kufafananua kuwa TMA imeshaanza kazi ya kuzihifadhi data za hali ya hewa katika mfumo wa kidigitali na kuahidi kuendelea kuifanya kazi hiyo kwa weledi, kwa upande wa ushirikiano na vyombo vya habari, Dkt. Kijazi alisema, hivi sasa Mamlaka inaushirikiano mzuri na mpaka sasa zaidi radio za kijamii 50 zinasambaza utabiri wa hali ya hewa unatolewa kila siku na hivyo kusaidia kuwa daraja la TMA na jamii. Vilevile, alitoa ufafanuzi kuhusu kuonekana kwa miji mingine katika vyombo vya habari vya kimataifa na miji ya Tanzania kutokuonekana, akisema ni utaratibu ambao upo ila suala hilo litafanyiwa kazi ili kuwekwa sawa.