Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania

ISO 9001:2015 Certified in Aviation Meteorological Services

Habari

 • AMCOMET Cairo, Egypt

  Imewekwa: 01st March, 2019

  Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye amezitaka wizara zinazosimamia sekta ya hali ya hewa katika nchi za Afrika kuhakikisha zinatoa ushirikiano wa hali ya juu kwa taasisi za hali ya hewa ili kufanikisha uboreshaji na utekelezaji wa majukumu yao. Nditiye alizungumza hayo wakati akihutubia mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya kusimamia sekta ya hali ya hewa barani Afrika, Jijini Cairo, Misri tarehe 21 Febrauari 2019 ulipofanyika mkutano wa AMCOMET-4.

  “Napenda kuweka msisitizo kuwa ni muhimu sana kwa Serikali zetu kupitia Wizara zinazosimamia sekta ya hali ya hewa katika nchi za Afrika kuhakikisha tunakuwa karibu na kuzisaidia taasisi za hali ya hewa zilizopo chini ya wizara zetu. Hii itasaidia katika kuboresha huduma za hali ya hewa na kurahisisha utekezaji wa majukumu yao kwa manufaa ya nchi zetu”. Alisema Mhe. Nditiye

  Aidha, Mhe. Nditiye alielezea namna ambavyo Serikali ya Tanzania imekuwa karibu na inasaidia Mamlaka ya hali ya hewa katika utendaji wake wa kila siku. Mhe. Nditiye alitoa mfano wa namna ambavyo Serikali ya Tanzania kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyosimamia na kufanikisha kupitishwa kwa sheria ya huduma za hali ya hewa mwezi Januari 2019 ambayo itaiwezesha TMA kuwa Mamlaka kutoka kuwa Wakala wa Serikali, kwa lengo hilo hilo la kuboresha huduma za hali ya hewa nchini Tanzania.

  Wakati huo huo katika mkutano huo Mhe. Nditiye alizungumzia juu ya umuhimu wa nchi kuwa na mpango mkakati wa Kitaifa (National Strategic Plan) unaohusu utoaji wa huduma za hali ya hewa ambao unaendana na mipango ya maendeleo ya nchi husika, huku akifafanunua faida za utekelezaji wake katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa kijamii na kiuchumi.

  Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes Kijazi alikuwa miongoni wa ujumbe wa Tanzania ulioshiriki katika mkutano huo wa AMCOMET-4 pamoja na Mkutano wa kumi na saba (17) wa wakuu wa Taasisi za hali ya hewa barani Afrika (RAI-17) uliofanyika pia Jijini Cairo, Misri kuanzia tarehe 22 hadi 23 Februari 2019, ambapo alipata kuungwa mkono kwa wingi na kwa hali ya juu sana na wakuu wenzake wa Taasisi za hali ya hewa barani Afrika kufuatia nia yake aliyoonesha ya kugombea nafasi ya makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ambayo iko wazi na uchaguzi na uchaguzi wa viongozi wa WMO utakaofanyika katika Mkutano Mkuu wa WMO (WMO Congress), Juni 2019.

  Mkutano wa AMCOMET-4 ulikutanisha washiriki mbalimbali kutoka nchi za bara la Afrika wakiongozwa na Mawaziri wenye dhamana ya sekta ya hali ya hewa au wawakilishi wao, Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kupitia Katibu Mkuu, Prof Petteri Taalas na Sekretariati ya WMO kanda ya Afrika, Wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa za nchi za Afrika, wataalamu mbalimbali wa hali ya hewa na washirika wa maendeleo kama vile Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo Barani Afrika (AfDB).

  IMETOLEWA NA MONICA MUTONI

  OFISI YA UHUSIANO

  MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

 • Weather by Region

  © 2019 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Haki zote zimehifadhiwa.